Wednesday, April 22, 2009

Mazingira yakituzwa huvutia watalii



Gladness Munuo


WATAFITI wa mazingira ulimwenguni, wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa utunzaji wa mazingira pamoja na kutaka umma uelewe au ujiepushe na uharibifu wa mazingira hasa katika maeneo ya bahari na pwani.

Lengo likiwa ni kuboresha biashara ya utalii na kuwavutia wageni wa nje na ndani kwa kufuata mfumo wa utunzaji wa mazingira (Ecotourism) katika maeneo ya pwani ya Bahari ya Hindi Ukanda wa Zanzibar.

Kutokana na ushindani wa kibiashara na hasa kwa upande wa vivutio mbalimbali vya asili kwa watalii ambao kwa asilimia kubwa wamekuwa wakiingizia nchi fedha nyingi pamoja na mataifa mengine kiwango kikubwa cha pesa za kigeni.

Hilo linachangiwa na uwepo wa hoteli nzuri za kitalii zilizojengwa pwani ya bahari zikiwemo hifadhi mbalimbali za wanyama na kumbukumbu za kihistoria ambazo watalii hujifunza.
Hata hivyo jitihada za makusudi za kuvutia zaidi watalii wanaoingia hapa nchini licha ya kuwepo kwa mtikisiko wa uchumi wa dunia, zinahitajika kuyahifadhi na kuyatunza zaidi maeneo hayo.
Maeneo ambayo kwa lugha ya kitaalamu hujulikana kama ‘Ecotourism,’ kwa kuzingatia mfumo halisi wa utunzaji wa mazingira asilia.

Sasa imekuwa desturi kwa kila sekta za utalii na mazingira kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha kuwa hifadhi zilizopo zinalindwa bila kuharibiwa na kujiingiza zaidi kwenye soko la kiushindani kutokana na ubora wake ili kuongeza kipato mara dufu.
Wahifadhi wa mazingira kwa maeneo ya wanyama wamekuwa wakiweka ulinzi na kutoa maelekezo kwa waishio jirani au wapita njia ili kuhakikisha maeneo hayo hayaguswi wala kuchafuliwa au kuingiliwa kwa namna yoyote ile.

Aidha, ndivyo ilivyo kwa hifadhi za bahari pamoja na pwani zake, wamiliki wa hoteli wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha maeneo hayo ambayo ni vivutio vikubwa kwa watalii mbalimbali yanaendelea kuwa vivutio kwa uasilia.

Awali ya yote neno uhifadhi wa mazingira masikioni mwa wengi lilikuwa lina maana ya maeneo yenye wanyama pori na misitu ya asili pekee.

Ni vema ikatambulika kuwa hata maeneo ya bahari na ukanda wa pwani yanahitaji uhifadhi mkubwa kwa ajili ya vivutio kwa watalii na wenyeji wanayoyazunguka.

Ni wazi kuwa wengi waliowahi kupata nafasi ya kufika maeneo ya pwani watakubaliana nami kwamba kutokana na wingi wa watu, maeneo mengi ya pwani ya bahari yamekuwa na matumizi mabaya ya mazingira yanayosababisha kuwepo na uchafuzi mkubwa wa mazingira.
Maeneo mengine kama vile pwani ya bahari yameonekana ni sehemu ya kutupiwa kila aina ya takataka bila kujali umuhimu wa maeneo hayo.

Leo hii juhudi kubwa zinafanywa na watu mbalimbali kama vile wadau wa bahari na pwani katika kuhakikisha hatua kali zinachukuliwa kwa kuweka ulinzi na nidhamu ambayo kila mkazi wa eneo hilo awe mtalii au mfanyabiashara ahakikishe suala la usafi wa mazingira pamoja na utunzaji ni mambo muhimu kwa maendeleo.

Naomba ieleweke kuwa uhifadhi wa bahari ni mpana, kwa maana ya kuwa upo uhifadhi wa mazingira ndani ya bahari na pwani.
Hatua moja wapo za kuhakikisha kuwa maeneo hayo yanaheshimiwa ni pamoja na kuwekwa kwa sheria mbalimbali za uhifadhi ikiwa ni pamoja na uvuvi wa kiwango maalumu kilichokubalika kitaifa na kimataifa katika kuhakikisha kuwa ongezeko la viumbe hai vilivyopo majini na nchi kavu vinalindwa.

Uhifadhi wa mazingira katika maeneo ya pwani pamoja na bahari kwa nchi za Afrika ni zana ngeni sana na imekuja kwa kasi baada ya ongezeko kubwa la watalii ambao bila ya kufanya hivyo basi pwani zetu zingekuwa zimeshavamiwa vya kutosha.

Kila mvamizi angefanya vile atakavyo na hivyo kuondoa ladha nzima ya eneo husika ikiwa ni pamoja na kutokuwepo kwa usafi au utunzaji wa mazingira halisi ambao ni kivutio kikubwa cha watalii.

Wingi wa watalii pamoja na wafanyabiashara mbalimbali umekithiri kwa kiasi kikubwa katika pwani zetu na hasa za Ukanda wa Bahari ya Hindi, hivyo kupelekea kuwepo kwa uharibifu wa maeneo na hali hiyo ikiendelea ni wazi kwa miaka ijayo hakutakuwa na vivutio halisi kwa watalii katika maeneo ya pwani.

Wamiliki wa hoteli katika pwani ya Bahari ya Hindi wameweka mkakati kuwa moja wapo ya hatua muhimu katika kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa ni kuanzishwa kwa utalii unaoendana na hali halisi ya kiuchumi na si utalii wa watu wengi bila ya kipimo ambao husababisha kuharibika kidogokidogo kwa mazingira husika.

Hii inadhihirisha kuwa elimu itolewayo na vyanzo husika, ikiwepo Taasisi ya Wanasayansi wa Bahari ukanda wa Bahari ya Hindi (Western Indian Ocean Marine Scientists Association -WIOMSA), wameweza kuwaelimisha kwa kiasi wadau wa Bahari ya Hindi na pwani kuzingatia kiwango kilichowekwa cha idadi ya watalii kwa uhifadhi salama wa mazingira utaowawezesha kuendelea kuwa na kivutio kwa watalii kwa miaka mingi zaidi.

Mfano halisi wa mazingira ya pwani yanayohifadhiwa kwa kuangalia hali hii ni pamoja na kisiwa kidogo cha Chumbe ambacho ni kati ya visiwa vidogo vilivyopo Zanzibar.
Kisiwani hiki, inasemekana, kina zaidi ya aina 300 ya viumbe hai mbalimbali viishiyo ndani ya maji na nchi kavu.

Ndani ya Kisiwa cha Chumbe yapo makazi maalumu yaliyojengwa kwa ajili ya watalii na watu mbalimbali ambao wangependa kwenda kushuhudia jinsi gani uhifadhi wa mazingira ulivyoimarishwa kiasi kwamba viumbe hai vilivyopo vinaendelea kuwepo bila kuathiri kwa hali halisi ilivyo.

Makazi hayo yaliyojengwa kiufundi kwa kutumia malighafi iliyopo hapo hapo kisiwani ni pamoja na ujenzi wa majumba makubwa 7 (Bungalows) ambayo ndani yake kuna vyumba vya kulala vilivyojengwa kwa kutumia malighafi ya asili.

Meneja Mradi wa kisiwa hicho, Frida Lanshammar, anasema utunzaji wa mazingira na matumizi ya vitu vinavyoendana kimazingira ni wa hali ya juu.
Anaeleza kuwa msisitizo unafanywa kwa kila mkazi au mgeni wa eneo hilo kutunza mazingira ikiwa ni pamoja na kutumia karatasi za chooni (Toilet paper) badala ya maji hasa wanapoenda kujisaidia; huku utayarishaji wa maji ya kunywa yasiyo ya chupa za plastiki yakisisitizwa.
Lanshammar ambaye ni raia wa Uingereza anasema makazi ya Kisiwa cha Chumbe kwa Pwani ya Afrika Mashariki ni ya kwanza na ya aina yake.

Kuna uhifadhi mzuri wa mazingira ulioonyeshwa katika makazi hayo na kujipatia sifa kubwa katika soko la utalii na kushinda kwa kiasi kikubwa kutokana na kuonyesha uhalisia wa hali ya juu katika mazingira yake.

Lanshammar alitoa maelezo hayo katika mafunzo ya waandishi wa habari wa Kenya, Tanzania na Seychelles waliopatiwa mafunzo ya uandishi wa mazingira katika maeneo ya Pwani ya Bara Hindi kama yalivyoandaliwa na WIOMSA wakishirikiana na Fojo –Taasisi ya mafunzo ya habari iliyopo nchini Sweden.

Makazi yaliyopo kisiwani Chumbe mbali na kuwa ni kivutio kikubwa cha watalii, vilevile imekuwa ni sehemu ya mafunzo kwa wanasayansi na wanafunzi mbalimbali.
“Watalii huweza kukaa kwa muda wa siku tano mpaka saba na gharama kwa watalii ni dola za kimarekani 100 kwa siku,” anasema Lanshammar.

Aidha, anasema kwa upande wa wanafunzi mara nyingi bei hupungua wakati mwingine huwa ni bure kabisa ili kuwawezesha kujionea na kuutangaza kwa nguvu zote utalii huo nje na ndani.
Kutokana na maelezo ya Lanshammar, ni wazi kuwa kulingana na hali halisi ya uchafuzi wa hali ya hewa kuna hatari maeneo hayo kukosa wageni na ndio maana ulinzi wa kutosha unakuwepo kwa kushirikiana na wananchi hali iliyoleta mafanikio makubwa.

Kwa upande wake, mwandishi wa habari za mazingira kutoka Sweden, Eva- Pia, anasema wanahabari wanapojifunza na kuandika zaidi habari za mazingira wataisaidia jamii kuwa mstari wa mbele kuyatunza na kujua umuhimu wake.

Eva-Pia anasema kuwa kurejesha uasili wa mazingira katika maeneo ya pwani za bahari kutasaidia viumbe hai waliopo kama samaki wasiathiriwe na wavuvi haramu na sehemu za mazalia mapya kuogezeka ili kuweza kukuza uvuvi wa kitalii katika maeneo hayo.

No comments:

Post a Comment