Saturday, June 28, 2014
MIGOGORO NA VURUGU HUIBUA UNYANYASAJI KIJINSIA KWA
WANAWAKE
• Azimio la Umoja wa Mataifa no.1325 lilete mabadiliko Tanzania
• Mabaraza ya Usalama kwa Vijiji, Kata, Wilaya na Mkoa washirikishe Wanawake
Na Gladness Hemedi Munuo
Imefika wakati wa nchi yetu Tanzania kupitia bunge letu tukufu kuridhia Azimio la Umoja wa Mataifa ya 1325 (UN Resolution 1325) ili kukomesha vitendo vya kikatili na unyanyasaji kijinsia wanavyotendewa wananchi wasiokuwa na hatia na hasa wanawake katika maeneo yenye migogoro.
Hii ni kwa kuwa, nchi zote zilizo katika Umoja wa Afrika Mashariki tayari zilikwisha ridhia Azimio hili la Umoja wa Mataifa na utekelezaji wake ili kukidhi haja za jamii zao. Iweje Tanzania mpaka leo tunasusua wakati tayari migogoro, vita na mashambulizi ya aina mbalimbali kwa jamii hivi sasa yameshamiri.
Uhalisia kamili umethibitisha kuwa, mahali popote panapotokea mgogoro, baina ya jamii kwa kutokuelewana kiasi cha kuzuka mapigano na uharibifu wa mali, vitendo vya unyanyasaji kijinsia vinavyojitokeza kama vile ubakaji kwa wanawake na watoto, utekaji nyara wa watoto wa kiume na wasichana ili waweze kuwatumikia watekaji kama watumwa au wake zao, pamoja na jamii hasa wanawake kuachwa wakiwa walemavu au kuharibiwa baadhi ya viungo vyao.
Azimio la Umoja wa Mataifa la 1325, linapinga kuwepo kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha kuwa wanawake wanahusishwa katika ngazi zote za maamuzi kuhusiana na kupatikana kwa amani nchini na duniani.
Vyombo vya habari vimekuwa vikijitahadi kuhabarisha umma kuhusu matukio dhalimu kama haya, lakini kwa uhakika wanao/walioathirika na majanga kama haya ni wengi, na kwa kuwa vyombo vya habari ni vichache vinavyoweza kufika vijijini na hasa maeneo yenye migogoro ili kuibua na kuhabarisha umma kikamilifu vitendo vya unyanyasaji kijinsia kwa jamii na hasa wanawake si rahisi habari nyingi kufika katika vyombo vya usalama kwa haraka.
Upo msemo unaosema ‘wapiganapo tembo nyasi ndizo zinazoumia’, pamoja na ‘Vita vya Panzi ni furaha kwa Kunguru’. Misemo hii inaashiria kuwa, wakati wowote tusikiapo ya kuwa kuna mgogoro wa aina fulani kiasi kupelekea jamii kukimbia makazi yao, wazee na wagonjwa huachwa bila ya msaada wowote aidha, wapo wakina mama wanaojifungulia maporini maeneo ambayo hayana usalama kiafya ikiwa ni pamoja na wanawake kufanyiwa vitendo vya kikatili kama vile kubakwa, kulawitiwa nk.
Hivyo basi, muarobaini wa athari hizi, ni kuwepo kwa maridhiano ya Azimio la Umoja wa Mataifa no.1325, ili utekelezaji wake uanze mara moja, huenda dawa ya kutokomeza migogoro hii ikiwa ni pamoja na kutibu itakuwa imekamilika kwa njia hii.
Asasi ya Wanawake katika mapambano ya amani Tanzania (TAWOPE), ni moja wapo ya taasisi yenye malengo ya kuhakikisha kuwa, jamii na wanawake waliopo katika maeneo yenye migogoro wanapatiwa elimu mbalimbali kama vile kujilinda na jinsi ya kujikinga miili yao kufuatia kuzuka kwa migogoro na vurugu za mara kwa mara, ufahamu wa sheria ya ardhi vijijini ya mwaka 1999 na elimu nyingine mbalimbali.
Mbali na TAWOPE, aidha zipo asasi ambazo zimejikita katika kutoa misaada mbalimbali kwa waathirika wa migogoro ya aina yeyote ile, ikiwa ni pamoja na ushauri nasaha kwa walioathirika kwa njia moja au nyingine, hizi ni asasi kama Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania (TAWLA), Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), na wengineo wengi.
Aidha, zipo asasi zinazotakiwa kuwa mstari wa mbele katika kushughulikia waathirika wa migogoro hiyo kama vile waliobakwa na kupata majeraha, ujauzito na hata maradhi mbalimbali ikiwemo UKIMWI, hawa huhitajika kupata msaada wa kiafya kutoka asasi husika kama vile Chama cha Madaktari wa Kike Tanzania (MEWATA), pamoja na asasi zenye kutoa huduma kama hizo.
Aidha, katika utafiti uliofanywa na TAWOPE (2010), ilionyesha kuwa katika nchi ya Tanzania maeneo ambayo kwa hakika migogoro isiyokwisha hujitokeza mara kwa mara, ni maeneo wanayoishi wafugaji na wakulima, na kikubwa hasa ni kwa wafugaji kuwa na idadi kubwa ya mifugo ambapo mara zote huingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima na kusababisha kuzua kutokuelewana kati yao na wakulima.
Ingawaje maamuzi ya UN ya 1325 yanalenga kulinda na kutetea maslahi ya wanawake hasa katika maeneo ambayo migogoro au vurugu zenye matumizi ya silaha zimejitokeza upande mmoja au pande zote.
Siyo siri kuwa, hata Tanzania, wananchi walio wengi wameshuhudia baadhi ya wafugaji wakitumia silaha ikiwa ni pamoja na bunduki zenye risasi za moto, ambazo madhara yake ni makubwa kwa jamii yote na hasa kwa wanawake ambao wamekuwa ndiyo kichaka cha uonevu. Je, mpaka leo tujiulize, Tanzania tunasubiri nini mpaka Azimio hili litupite?
Vurugu au migogoro ya hivi karibuni jamii imeweza kushuhudia wakati wa Operesheni mbili za kitaifa (Tokomeza na Kimbunga), kumekuwa na vitendo vya ubakaji na kila aina ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na wanaume waliokumbwa katika hizo operesheni ambazo ziligeuka na kuwa ni vurugu kwa jamii husika.
Mfano halisi wa wanawake walioathirika ni pale ambapo baadhi yao wamelazimika kuolewa kinguvu na wafugaji au askari wanaosimamia operesheni mbalimbali kama tulivyoshuhudia nchini Tanzania hivi karibuni.
Taarifa kama hizi zinasimuliwa na waathirika wenyewe katika maeneo ya Mahenge –Itete, Morogoro- Mvomero, Loliondo na Manyara. Aidha, Mara-Tarime, Pwani –Rufiji pamoja na maeneo mengine ambayo wafugaji wameingia kwa wingi.
Angalizo pia tunatoa kwa serikali yetu, katika kipindi hiki ambacho wananchi wanajiandaa na uchaguzi wa taifa, zipo dalili ya kujitoza kwa vurugu za kisiasa ambazo kwa Tanzania tumeshashuhudia baadhi ya vifo mfano mauaji ya mwandisha wa habari huko Iringa, aidha vurugu za silaha za moto (bomu) kwa raia wasiokuwa na hatia katika nyumba za ibada Zanzibar na Arusha, na hata katika mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa..
Kipindi hiki Tanzania inapoandaa Katiba Mpya, ndiyo wakati muafaka wa kuhakikisha pia Azimio la Umoja wa Mataifa no.1325 linazingatiwa kwa kuridhia na kuhalalisha utekelezaji wake ili migogoro iliyopo na inayoendelea kujitokeza iweze kudhibitiwa.
Hivyo basi, mapambano dhidi ya vitendo vya unyanyasaji kijinsia yanahitaji ushirikiano kutoka serikalini, asasi zote zenye kuunga mkono haki za binadamu pamoja na vyombo vya habari katika kuhabarisha jamii.
• Mwandishi Gladness Munuo ni Mratibu wa Asasi ya Jinsia na Vyombo vya Habari, Tawi la Tanzania.
0754/0786/0754 285701
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment