Na
Dominica Cassian Haule
Ukatili wa kijinsia ni msemo mpana sana.
Unagusa binadamu wote wanawake na wanaume. Lakini ni ukweli usiopingika kwamba
ukatili wa kijinsia unawaathiri kwa asilimia kubwa wanawake na wasichana kuliko
ilivyo kwa wanaume na wavulana. Kuna tafiti lukuki zinazothibitisha.
Wakati wa mababu na mabibi zetu, tulisikia
mwanamke kapigwa, kavunjwa mkono, kauawa na kadhalika na kadhalika. Tuliongozwa
na tamaduni na kuona maisha ndivyo yanavyotakiwa kuwa.
Raia yenye furaha ni hazina kwa taifa |
URITHI
Binafsi, nashawishika kuamini kuwa, ukatili
wa kijinsia, umekuwepo tokea mwanzo wa uzao wa binadamu. Ukipitia maandiko
mbali mbali, utakuta maandiko, mtu na mkewe. Kwa hili mimi na wewe hatuna budi
kujiuliza, hivi mtu ni nani?.
Lakini pia katika maandiko hay ohayo,
utakutana na semi binadamu wote. Basi, na tubadilike, tukijua kuwa kwa kuwa
neno binadamu wote inamaanisha watu, kwa hiyo, watu hao ni wanawake na wanaume.
Katika familia zetu, kilio kikubwa bado
kinaumiza mabinti pale ambapo wazazi/walezi wanapogawa majukumu fulani kuwa ya
wasichana na mengine kuwa ya wavulana. Mara nyingi inasahaulika kuwa, vyovyote
iwavyo, majukumu ya wasichana yanaweza kuchukua asilimia kubwa ikilinganishwa
na asilimia ya majukumu ya wavulana.
Japo kwa asilimia fulani, wakazi wa mijini
wameweza kutambua umuhimu wa kuwapa watoto wao majukumu yanayofanana ili mradi
hayavuki mipaka. Hii ni njia mojawapo ya kutoa malezi endelevu kwa watoto wote
wa kike na wa kiume.
Kadhalika tumeshuhudia, wazazi wanaojadili
kutegemea uzao wa watoto wa kiume tu. Na haya yanapatiwa baraka na wanawake
pia. Fikiria mama mjamzito anapolazimika
kuomba ajaliwe mtoto wa kiume.Lakini sio kwa matashi yake, bali kwa matashi ya
jamii inayomzunguka. Imemtengenezea mtizamo wa kuthamini mtoto wa kiume japoku
yeye ni mwanamke.
HABARI SAHIHI
Vyombo vya habari kwa ujumla wake navyo
vinachangia kwa kasi kuwanyima uelewa mpana wananchi ili waachane na vitendo
vinavyochangia ukatili wa kijinsia. Haviandiki au kutangaza kwa undani yale
yanayopinga ukatili wa kijinsia, ili wananchi wapate upembuzi yakinifu.
Kwa mujibu wa jarida, Jinsia na Vyombo vya
Habari Tanzania, lililobeba stadi juu ya mwendelezo wa jinsia na vyombo vya
habari (2010), sauti za wanawake
zinasikika pale tu habari inapohusu ukatili wa kijinsia na usawa wa kijinsia.
Ambazo zinachukua asilimia 71 na 67. Na habari hizo ni zile za udhalilishaji,
mfano ukahaba, mauaji ambayo yametendwa na mwanamke na kadhalika.
Ingefurahisha na kupongezwa iwapo habari hizo
zingekuwa zile zinazoleta maendeleo kwa nchi, ukizingatia kwamba asilimia 70 –
75 ya kazi za uzalishaji hasa sehemu za vijijini hufanywa na wanawake.
La kusikitisha, habari zinazohusu madini
kwa mujibu wa jarida hilo hazikupata nafasi katika vyombo vyetu vya habari.
Sambamba na hizo, zile zinazohusu ajira
zilipata fursa kwa asilimia kumi tu na zile zinazohusu makazi zilipatiwa nafasi kwa asilimia kumi kadhalika.
Stadi juu ya mwendelezo wa jinsia na vyombo
vya habari Tanzania iliyoratibiwa na asasi isiyo ya kiserikali ya Jinsia na
Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania – GEMSAT kwa ufadhili wa asasi isiyo ya kiserikali yenye makao makuu
nchini Afrika kusini –‘ Gender Links’, imebaini
pia kwamba asilimia sita (6) ya wanawake hubeba utambuzi wa mama, mke au binti
kwa upande wa chanzo cha habari. Wakati asilimia nne tu (4) ya wanaume hubeba
utambuzi wa baba, mtoto wa kiume au mume.
Hili lina maana gani kwetu. Ni kwamba,
mwanamke au msichana bado anatambuliwa
kupitia kwa baba yake mazazi/mlezi au kupitia kwa mumewe.
Japokuwa ukatili wa kijinsia umebainika
kufanyika kwa kiwango cha kutisha si tu nchini Tanzania, bali hata katika
nchini zilizopo kusimwa mwa Afrika, ni asilimia tatu tu (3) ya habari
zinazoandikwa na kutangwa zinaongelea ukatili wa kijinsia.
HISTORIA
Kwa mujibu wa kitabu WANAWAKE WA TANU (Jinsia na Utamaduni katika Kujenga Uzalendo
Tanganyika: 1955 – 1965),”wanawake wazalendo walikuwa ni viongozi mashuhuri
katika medani zote kwenye ngazi mbalimbali. Wanachama wengi wa TANU walikuwa wanawake na walihusika na
majukumu ya kuchangisha fedha, uhamasishaji wa nyumba hadi nyumba na ushawishi
wa wanachama katika makundi mbalimbali.”
Kitabu hiki ambacho mwandishi wake ni Susan
Geiger, kimetafsiriwa na kurahisishwa na Elieshi lema kwa niaba ya Mtandao wa
Jinsia Tanzania (TNGP), kwa lengo
mahsusi kuwakumbusha Watanzania na wale wote wanaojali na kuheshimu utu,
kutambua kuwa nafasi ya wanawake katika jamii haipaswi kudharauliwa, kubezwa na
hata kukejeliwa kwa visingizio mbalimbali. Hili linapotendeka, huu ndio haswa,
unyanyasaji kijinsia.
Kitabu hiki kilichosheheni visa mkasa
lukuki kinaeleza kwa kina wanawake hawa wazalendo walivyojenga uelewa wa ni
nini maana ya utaifa kunzia TANU.
Kwa
mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania ( TAMWA juu ya ujanyanyasaji wa kijinsia, hali bado
ni mbaya. Hali hii ina maana gani kwa serikali, wanaharakati, wanahabari
kadhalika Watanzania kwa jumla.
Hii
inataka jitihada za ziada katika ngazi zote kuanzia serikali za mitaa hadi
serikali kuu.
Mwaka
2011, nilisafiri kwa basi toka kituo
kikuu cha mabasi ya abiria yaendayo mikoani cha Ubungo jijini Dar es Salaam,
kuelekea wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
Kama kawaida ya safari za mikoani, basi
hilo likiwa limeenea abiria katika viti vyote, liliondoka katika kituo hicho
saa 12.30 asubuhi.
Baada ya mwendo mathalani wa saa mbili,
nakumbuka mama mwenye mtoto wa kike mwenye umri kama miaka mitano, alimfuata
kondakta na kumweleza kuwa mtoto alihitaji kujisaidia.Kwa mujibu wa mama
huyo alijibiwa asubiri kidogo.
Nakumbuka vizuri kwamba basi lilipamba moto
hadi tukafika sehemu ya kuongeza mafuta. Mama yule ambaye alilazimika kurudi
katika kiti chake baada ya kuambiwa asubiri, alimjongelea tena dereva
kumkumbusha nia yake ya kumpeleka mtoto ajisaidie.
Huwezi kuamini kwamba dereva alimkatalia yule
mama na kuendelea kuchanja mbuga. Kilichofuatia ni ukulele mzito toka kwa kina
mama waliokuwa ndani ya lile basi. Amini usiamini, dereva alilazimika
kusimamisha basi na mama yule kumpeleka mwanaye nje ili ajisaidie.
Ukatili kama huu uleta kilema cha maisha. |
Hii kama haitoshi, kina mama ndani ya basi
lile kwa umoja wao, walimlaani dereva kadiri kila mmojawao alivyojaliwa na
muumba wake. La kushangaza, kina baba walifumba midomo yao kana kwamba
hawakusikia wala kuona kilichokuwa kikiendelea baina ya dereva ambaye ni
mwanaume mwenzao na mama wa mtoto.
Niliwaza sana na kuwazua kuhusu hili,
nikaogopa sana kuhusu maisha yetu iwapo katika kipindi hiki miaka zaidi ya
hamsini tokea tujitawale bado tu kina baba hawana uchungu wa kuona kwamba mama
awaye yeyote ni sawa sawa na mama yako.
Kadhalika,umwone mtoto wa mwenzio, jirani, rafiki kuwa ni mwanao.
Kutoka Sengerema, kurudi Dar es Salaam
nikiwa katika basi tofauti na lile la awali, nilishuhudia kituko kingine kutoka
kwa dereva wa basi hilo.
Baada ya mwendo wa karibu kutwa nzima.
Majira kama ya saa nane au tisa mchana, aliruhusu abiria kuchimba dawa
(kujisaidia) wakati yeye akiongeza mafuta katika basi. Lakini sehemu hiyo
ilikuwa na choo chenye vyumba viwili tu. Kimoja kwa wanaume na kimoja kwa wanawake.
Hilo kama halitoshi, ni sehemu ambayo mabasi mengi husimama kuongeza mafuta na
abiria kuchimba dawa (kujisaidia).
Nakumbuka wakati huo kulikuwa na mabasi
takribani matatu. Fikiria abiria wangapi walihitaji huduma hiyo kwa wakati
mmoja. Kilichotokea ni kwamba, wanaume kwa jinsi Mungu alivyowajalia, waliweza
kujificha ficha na hivyo kuwahi kwenye mabasi kabla ya wanawake.
Hali hiyo ilisababisha wanawake washindwe
kujikamilisha kabla ya muda ambao ulitolewa. Dereva wa
basi nililopanda akaondoa basi bila ya kujali kuwa, kuna wanawake
walikuwahawajaingia licha ya kuelezwa. Kama kawaida akapigiwa kelele na
wasamaria wema na kutishiwa kuwa wangempiga laiti angewaacha kina mama hao.
Visa mkasa hivi viwili, ni vionjo tu
nilivyokupa ndugu MTANZANIA. Katika
kisa mkasa cha mwanzo, unaona wazi ni jinsi gani ukatili wa kijinsia unavyotesa
wanawake. Mama huyu na mwanae wa kike wote wameangukia katika lindi la
kufanyiwa ukatili.
MTANZANIA mwenzangu ni mara ngapi tumeshuhudia tukiwa safarini, wanaume
wanavyowaomba madereva wasimame ili wajisaidie. Tena, kila wanapojisikia, wala
hawajali kama ni mahali pa wazi au penye usiri.Tena wako baadhi ya madereva,
wanaotumia fursa za wanaume kuwasimamisha
mara kwa mara, kuwapa pia fursa
hiyo abiria wengine, bila kujali kuwa sehemu husika haitawafaa wanawake. Huu ni
UKATILI WA KIJINSIA.
Kisa mkasa cha pili, kadhalika. Ni wajibu
wa madereva kuhakikisha kuwa sehemu wanazowapeleka abiria wao ‘kuchimba dawa’
zinakidhi mahitaji ya wanawake na wanaume kwa wakati mmoja?. Iwapo hazikidhi,
basi watafute maeneo ambayo hayatakuwa ya
karaha hususan kwa wanawake na wasichana.
Jambo lingine kubwa na la msingi ni kwamba,
mara nyingi wasafiri hawa huandamana na watu wanaowaheshimu. Ambao kwa mujibu
wa tamaduni zetu, hawawezi wakaandamana nao ‘kuchimba dawa’ katika eneo moja.
Lazima mmoja awe mbali na mwingine. Mfano, mama amesafiri na babake mzazi/baba
mkwe. Au mtoto mwenye umri mkubwa amesafiri na mama yake mzazi/mama mkwe.
Katika haya, WATANZANIA wenzangu
tusidanganyane kwamba tunakwenda na wakati. Haya hayana wakati, tumezaliwa
tumeyakuta na tutaendelea kuyaenzi kwa faida ya vizazi vijavyo.
Dominica
Cassian Haule, ni Mwandishi wa Habari / Mchambuzi wa Masuala ya Jinsia na Mwenyekiti wa Asasi ya Jinsia na Vyombo
vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania – GEMSAT.
dominicahaule@yahoo.com
No comments:
Post a Comment