Thursday, September 24, 2009

WANAHARAKATI WA JINSIA NA KAULI YA PELEKA RASILIMALI KWA WANAWAKE WALIOKO PEMBEZONI

Wanawake wanaharakati wa Jinsia kutoka asasi mbalimbali nchini wakiwa kwenye moja ya vikao vya matayarisho ya Tamasha la Jinsia Tanzania hivi karibuni, kikao hicho kilifanyika katika ofisi za Asasi ya Jinsia Tanzania (TGNP, Septemba,2009)
Mary Rusimbi, Mkurugenzi Mtendaji wa kwanza wa TGNP akisimamia shughuli za matayarisho ya Tamasha la Jinsia katika moja wapo ya vikao vyake hivi karibuni.

Gladness Hemedi Munuo
GEMSAT


- Watanzania na wanaharakati wanaadhimisha Tamasha la 9 la Jinsia;
- Kauli mbiu imetolewa wakati muafaka;
Nayakumbuka maneno ya mwanaharakati mkongwe wa masuala ya jinsia nchini Tanzania Charles Kayoka Mwandishi mwandamizi ambaye alishiriki katika kuazimisha miaka 20 ya Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), na nukuu “ Wanaharakati kwa ujumla pamoja na wana TAMWA wasing’ang’anie kutekeleza yale mambo muhimu machache yaliyo kwenye mpango kazi wao pekee, au mipango wanayopangiwa na wafadhili mbalimbali au iliyokwisha andaliwa na serikali tayari, bali wawe na mbinu zao za kubuni ikiwa ni pamoja na kufanya tafiti kwa umakini kwa kuwashirikisha wanaharakati na wataalamu waliobobea katika fani mbalimbali.”

Nimeyakumbuka maneno haya wakati huu wa maadhimisho ya tisa (9) ya Tamasha la Jinsia Tanzania ambalo limeandalliwa na wanaharakati wa masuala ya jinsia nchini (FEMACT) wakishirikiana na asasi ya masuala ya jinsia Tanzania –TGNP.
Asasi ya TGNP au kama inavyojulikana na wengi “Tanzania Gender Networking Programme” ilianza rasmi kama asasi kamili toka mwaka 1993. Baadaye kwa usimamizi wake waliweza kuunda umoja wa asasi zinazojishughulisha na masuala ya jinsia (FEMACT) ili kuweka nguvu ya ziada kuhakikisha kuwa kile kinachofanyiwa kazi kiweze kupata nguvu katika utekelezaji wake ikiwa ni kwa ngazi ya wilaya, mkoa au Taifa.
Harakati za TGNP pamoja na FEMACT zinanikumbusha haswa maneno ya mwanaharakati wa masuala ya jinsia Charles Kayoka ambapo ukiyachambua kwa umakini unaweza kupata jibu la uhakika kuwa si rahisi kwa asasi moja pekee ikafanikiwa kwa kiasi cha kuridhisha pasipo kushirikiana na asasi nyinginezo zenye mrengo sawa, serikali alikadhalika wataalamu au wasomi wa masuala mbalimbali.
Hii ndiyo iliyopelekea TGNP ambayo ilianza rasmi mwaka 1993 kuona umuhimu wa kushirikisha wanaharakati wa asasi nyinginezo na kuunda umoja ujulikanao kama FEMACT. Hivyo basi, kwenye mchangamano huo unao wataalamu wa fani mbalimbali lakini wote wakiwa malengo yanayolingana.
Hivyo basi, kutokana na ushirikiano huo, umewezesha kuwepo kwa Tamasha la Jinsia nchini Tanzania ambapo linaungwa mkono na watanzania wote kwa ujumla, taifa la Tanzania na kimataifa. Maadhimisho hayo ambayo hufanyika kila baada ya mwaka mmoja ili kutoa muda wa kutosha katika kufuatilia yale yaliyoazimiwa kwa pamoja na wana FEMACT ikiwa ni pamoja na wananchi wengine wote walioweza kushiriki wakati wa Tamasha.
Katika kuhakikisha kuwa Tamasha la Jinsia nchini Tanzania linawashirkisha watanzania wote kwa makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja watoto, walemavu wa aina mbalimbali, wazee nk. Hii ni kuhakikisha kuwa mshikamano katika maamuzi au kampeni mbalimbali unajumuisha madaraja ya watanzania wa aina zote.
Mkurugenzi wa Asasi ya Jinsia Tanzania (TGNP) Bibi Ussu Malya alisema kuwa, “Madhumuni makubwa ya Tamasha la jinsia nchini mwetu kwa kila muhula ni kuwakusanyisha wanawake na wapenda harakati za wanawake pamoja na wananchi wote wenye kujali usawa wa jinsia na hasa masuala ya wanawake katika ngazi mbalimbali za maisha ikiwa ni vijijini, wilayani pamoja na pande zote za dunia, kwa malengo ya uanaharakati katika kutoa habari na kubadilishana mawazo katika masuala muhimu”.
Kutokana na mchakato huo ambao Bibi Ussu ameufafanua kwa undani, ndiyo nguzo muhimu inayosimamiwa katika kufanikisha kuwa Tamasha la Jinsia nchini Tanzania linafanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Kubadilishana kwa mawazo miongoni mwa washiriki mbalimbali wa kutoka ndani na nje ya nchi hukamilisha safu ya kubadilishana mawazo na uzoefu wa kazi mbalimbali za kiuhanaharakati nchini.
Wataalamu, wasomi na wazoefu wa mazingira ya jamii na dunia kwa ujumla aidha wamekuwa chachu kubwa katika kuhakikisha kuwa Tamasha la Jinsia Tanzania linafanikiwa si tu kwa kushirikisha watu mbalimbali na kufanikiwa bali pia kuhakikisha kuwa mada muhimu zitakazo zungumzwa na washiriki zinafuatiliwa kwa ukaribu ili serikali iweze kutilia mkazo utekelezaji wake.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni “ Tupeleke Rasilimali kwa Wanawake walioko Pembezoni”, ujumbe huu kwa nyakati kama hizi na mambo yanavyotendeka ni muhimu sana katika kupigiwa kampeni ya kutosha. Umefika wakati serikali ikaliangalia suala hili kwa jicho la ziada.
Kutokana na idadi ya watu waliopo Tanzania, tunaelezwa kuwa asilimia kubwa ya wakazi wako vijijini, kwa maana hiyo wanawake walio wengi wako huko vijijini. Hiyo haina mjadala, kwa maana hiyo moja kwa moja hatuna budi kuwapongeza wana FEMACT kwa kuchagua kauli mbiu muhimu kama hii ambayo kwa zama hizi suala hili ni muhimu sana.
Imeshasemwa mara nyingi sana kuwa mijini ndiko kwenye kila kitu muhimu kwa binadamu kama vile mashule, hospitali au vituo vya afya, magulio ya kuuzia mazao n.k. Kutokana na hilo imekuwa ni nadra kuona maendeleo muhimu kama hayo yakiongezeka kwa kasi katika maeneo ya vijijini au pembezoni.

Wana FEMACT wameona awamu hii, suala hili lipigiwe debe la kutosha ili serikali na asasi nyinginezo ziweze kuchukua hatua na utekelezaji ufanyike haraka iwezekanavyo ili wananchi wa Tanzania waweze kurudisha imani yao kwa serikali yao.
Katika nchi yetu ya Tanzania hatuna budi kuwapongeza asasi binafsi, watu binafsi mmojammoja pamoja na mashirika ya dini kwa jinsi walivyoweza kujidhatiti kuanzisha shule za ufundi, vyuo vya maendeleo na hata vituo vya afya ambavyo ndivyo vinawakomboa wananchi wengi waliopo pembezoni.
Ni jambo la fedheha sana mpaka sasa ni muda wa miaka 48 toka nchi yetu ijipatie uhuru wake kwa njia ya amani lakini mpaka leo hii bado jamii iliyoko pembezoni na hasa wanawake hawana mahitaji muhimu hasa huduma za afya na kusababisha kuwepo kwa ongezeko la vifo vya uzazi kwa wanawake.
Umefika wakati kwa huduma muhimu ziegemezwe pembezoni walipo wananchi wengi na wapiga kura wakutegemewa, huduma kama mabenki mfano Benki mpya ya Wanawake ilyozinduliwa tarehe 4 Septemba, 2009 na Rais wa Jamhuri Mheshimiwa Jakaya Kikwete, Benki kama hii ambayo imeanzishwa wakati muafaka ingekuwa vema ikafungua matawi kwa wingi huko wilayani ili kuweza kuwakwamua wananchi wengi na hasa wanawake waliopo huko ambao ndiyo tegemeo la nguvu kazi kwa taifa hili.

Hongereni sana wana FEMACT kwa kuja na dira nzuri yenye mwelekeo wa maendeleo kwa taifa letu. Idumu TGNP! Idumu FEMACT! Wadumu wanawake wanaharakati wa Tanzania!
*GEMSAT ni Asasi ya Vyombo vya Habari na Jinsia Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania.
http://www.gladnesshemedi.blogspot.com/
+255 655 285701


A.Wanawake wanaharakati wa Jinsia kutoka asasi mbalimbali nchini wakiwa kwenye moja ya vikao vya matayarisho ya Tamasha la Jinsia Tanzania hivi karibuni, kikao hicho kilifanyika katika ofisi za Asasi ya Jinsia Tanzania (TGNP)

B.Mary Rusimbi, Mkurugenzi Mtendaji wa kwanza wa TGNP akisimamia shughuli za matayarisho ya Tamasha la Jinsia katika moja wapo ya vikao vyake hivi karibuni.