Saturday, June 28, 2014

VYOMBO VYA HABARI VYA KIJAMII - Toeni elimu kwa jamii madhara ya unyanyasaji kijinsia Na Gladness Hemedi Munuo Vyombo vya habari vya kijamii (Community Media) vikitumika sawasawa katika kutoa habari vitajenga na kuwa msaada mkubwa wa maendeleo kwa jamii katika kuelimisha madhara yanayokuwa kwa kasi sana ambayo ni unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake, watoto na wazee. Zipo jamii nyingi sana Afrika na hususan Tanzania ambazo mila na desturi huwageuza wanawake kuwa ni viumbe duni visivyo na sauti na hata kutofaa kustahili kuwa na haki. Na wahanga wakubwa wa mila na desturi zenye mfumo dume ni wanawake na watoto ambao kukandamizwa kwao kunatafsiriwa kama ni jambo la kawaida kwa jamii. Mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda ambayo nchi ya Tanzania kupitia bunge letu tukufu imeridhia, imeeleza kwa undani kuhusu uwajibikaji wa jamii na taifa kwa ujumla katika kuhakikisha kuwa mwanamke na mtoto analindwa na kuheshimiwa kama ilivyo kwa mwanaume. Hivi karibuni katika mkutano mkuu wa kwanza na kongamano kwa vyombo vya habari vya kijamii (Redio za jamii) uliofanyika mjini Bagamoyo, mambo mbalimbali yalijadiliwa katika kuhakikisha kuwa vyombo vya habari vya kijamii vinaimarika na kuwa msaada muhimu kwa jamii iliyovizunguka hasa katika kuelimisha kuutoko,eza unyanyasaji. Naweza kusema kuwa, kwa jinsi kasi ya manyanyaso, uonevu na ukatili kwa wanawake na watoto unavyopamba moto siku hadi siku, wapo wataalamu mbalimbali waliotoa ari kuwa vyombo vya habari vya kijamii viwe ndiyo nguzo kubwa katika kutoa elimu kwa jamii, kwa kuwa mpaka sasa ndivyo vyombo vinavyofanya kazi kwa niaba ya jamii na karibu na jamii (Cabrella-Balleza,M.’Community media by and for women’;AMARC women’s International Network, 2007). Majadiliano hayo yalilenga katika kuona kuwa vyombo hivi ambavyo kwa ujumla takribani kwa idadi vipo zaidi ya vyombo 20 walihudhuria kongamano hilo, walitoa ari kwa vyombo hivyo viwe na manufaa kwa asilimia 100 kwa wana jamii, ikiwa ni msaada katika kuondoa kero zilizopo pamoja na kuelimisha na kuburudisha. Suala moja wapo lililowekewa mkazo ni kuhakikisha kuwa vipindi vyote vya redio viandaliwe katika mfumo wa kuhakikisha vinakidhi matakwa ya jamii zote na zaidi wanawake na watoto ili kwenda sawa na ‘Protokali ya Jinsia na Maendeleo katika kanda ya kusini mwa Afrika’. Ambayo katika kifungu cha 29-31kinazungumzia masuala ya habari, taarifa na mawasiliano na msisitizo ni kuwa ifikapo mwaka 2015 masuala ya jinsia katika vyombo vya habari yatakuwa yameshika kasi nzuri kutokana na mafunzo mbalimbali yanayotolewa kwa waandishi wa habari, aidha sera za jinsia zitaendelea kuwepo na kuhamasisha waandishi katika kutetea masuala ya jinsia. Sio jambo geni kwetu tunaposikia taarifa mbalimbali kupitia vyombo vya habari zikituhabarisha matukio ya unyanyasaji kwa wanawake na watoto yanavyokuwa siku hadi siku, na ndiyo maana msisitizo umetolewa katika kuhakikisha vyombo vya habari vya kijamii kuweka agenda ya mkakati wa kutoa elimu hii kwa umma. Katika kongamano la kwanza kwa vyombo vya habari vya kijamii, kero za unyanyasaji wa jinsia kwa jamii ilionekana kushika kasi hasa kutokana na takwimu sahihi kama zinavyoainishwa na ‘Tanzania Demographic and Health Survey (TDHS)’ ya mwaka 2010. TDHS inaonyesha kuwa unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto wa kike ambao hawana ndoa ni asilimia 44% wakati wanawake walio katika ndoa ni asilimia 20. Ikumbukwe kuwa hizi ni takwimu kwa matukio yaliyotolewa taarifa katika vituo vya polisi na mahospitalini, na penginewe ni sehemu za mijini tu. Kwa maana kwamba zipo taarifa nyingi za matukio kama hayo katika maeneo ya vijijini na zaidi ambazo hazijajulikana. Hii ni kutokana na wana familia na jamii kuamua kuyafumbia macho matatizo kama hayo na kuyageuza kama jambo la kawaida katika familia. Katika kuchangia mada hii, mwakilishi kutoka katika Redio ya Jamii Kigoma, alielezea masikitiko yake kuhusiana na haki ya watoto kielimu inavyoporomoka kiasi kusababisha watoto wa kike kukosa elimu kwa kupata ujauzito wakiwa mashuleni. Naye mshauri wa redio/vyombo vya habari vya kijamii kutoka UNESCO Bi Rose Haji alielezea umuhimu wa sera za jinsia na vyombo vya habari zinavyopaswa kufanyiwa kazi kwa vitendo, ikiwa ni pamoja na uandaaji wa vipindi, muda wa kurusha vipindi hewani kulingana na ratiba au desturi za kila siku za jamii husika. Jambo lililopongezwa katika kuhakikisha kuwa itakuwa ni rahisi kwa habari lengwa kufika kwa walengwa bila pingamizi, ni kuwepo kwa matumizi ya lugha ya Kiswahili ambayo mpaka sasa imani kubwa ni kuwa watanzania walio wengi lugha hii wanaifahamu na hasa kwa kusikia na kuelewa hata kama hawatazungumza. Hivyo basi, wito ulitolewa kwa wanahabari wa vyombo vya kijamii kutumia vyombo vya habari ikiwa pamoja na kalamu zao kama vitendea kazi katika kuhakikisha kuwa jamii inatambua madhara ya unyanyasaji yaliyopo kwa upande wa wanawake na watoto. Washiriki na wajumbe katika kongamano hilo walijadili kwa kina ya kuwa njia nzuri ya kufikisha ujumbe kwa walengwa (wasikilizaji) ni kuwepo kwa hatua za awali katika kuhakikisha hilo linatekelezeka kwa kuwajengea uwezo waandaaji na wapelekaji wa habari hizo kwa jamii kupitia vyombo vya habari vya jamii. Elimu kama hii imekuwa ikitolewa na asasi kama vile Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Asasi ya Jinsia na Maendeleo ya Vyombo vya Habari Tawi la Tanzania (GEMSAT), Baraza la Habari Tanzania (MCT) nchini na vimekuwa mara zote vikiwalenga zaidi waandishi wa habari wa vyombo vya habari vya kawaida na kuwasahau waandishi waliopo katika vyombo vya habari vya kijamii. Kongamano hilo ambalo liliendeshwa kwa siku tatu, lilionyesha imani kubwa kuwa, vyombo vya habari vya kijamii vikiwezeshwa kisawasawa, basi litakuwa daraja muhimu katika kuirekebisha jamii au kuondoa kabisa kero za unyanyasaji wa kijinsia kwa jamii. Ukitaka kujua ni kwa vipi wanawake na watoto wananyanyasika kijinsia, tembelea katika vituo vya polisi vilivyopo katika maeneo ya makazi ya watu. Aidha pita katika hospitali na vituo vya afya upate kujionea visa mkasa na madhila yanawapata wanawake walio wengi. Aidha mila nyingi za jamii mbalimbali nchini Tanzania zinaongeza a na kuona kama ni sehemu ya maisha na mwanamke hana sauti ya kujitetea. Aidha, wapo wale wanaodhani kuwa, desturi ya ukandamizaji na uonevu kwa jinsia isiyo na sauti (wanawake) ni jambo sahihi au suala la kawaida. Wito umetolewa kwa wamiliki wa vyombo vya habari vya kijamii kuvalia njuga elimu ya kukomesha unyanyasaji kwa wanawake na watoto. Suala hili likitiliwa mkazo mafanikio yataonekana. Tushike maneno ambayo Hayati baba wa taifa hili muasisi wa serikali yetu na Rais wa kwanza wa Tanzania Mheshimiwa Julius Kambarage Nyerere, ambaye aliwahi kusema kuwa ‘inawezekana ikiwa kila mmoja atatimiza wajibu wake’. Gladness H. Munuo: Ni Mratibu wa Asasi ya GEMSAT Mobile No.+255 754 285701

No comments:

Post a Comment