Wednesday, February 18, 2009

Valentine iwe siku ya kudumisha upendo kati ya ndugu

Mwezi Februari wa kila mwaka au kama unavyojulikana kwa walio wengi mwezi mzuri wa wapendanao, nchini Tanzania kama ilivyo katika nchi nyinginezo barani Afrika na Ulaya kote si haba kuona pilika pilika kwa vijana na wazee, watoto na wazazi wao, ndugu kaka na dada, mke na mume na hata wachumba au marafiki kila mmoja kwa wakati wake akitafuta vitu kama maua, zawadi na mishumaa ya rangi kwa ajili ya kusherehekea kilele cha siku ya wapendanao ambayo ni tarehe 14 ya kila mwezi wa 2 kwa kila mwaka. Mwandishi wa kujitegemea Gladness Hemedi Munuo wa Taasisi ya Jinsia na Habari kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania, anafafanua zaidi…..


Imekuwa ni jambo la kawaida kabisa sasa hivi kwa Watanzania waishio sehemu za mijini kutakiana heri ya ‘wapendanao’ kwa wiki nzima kabla ya siku yenyewe husika, ambapo siku ya kilele shamrashamra, shangwe na bashasha huzidi kipimo kwa jinsi wapendanao wanavyoonyesha upendo kati yao kwa njia mbalimbali. Katika Lugha ya kiingereza hujulikana na wengi kama “Valentine Day”.

Siyo siri kwani kwa karne hii Valentine Day inashabikiwa sana na kundi la vijana pamoja na wazee, ushabiki unaonekana waziwazi pale ambapo wapendanao hao au wale wanaoiadhimisha siku hiyo wanapokuwa na kivazi rasmi kwa siku hiyo ambacho ni nguo zenye rangi nyekundu au wekundu na pinki ili mradi tu rangi nyekundu ambapo hufananishwa na ua rose inaonyesha upendo.

Siyo ajabu kuona hata kwa siku za kawaida kijana au baba au msichana au mama akichukua ua jekundu na kumkabidhi ampendaye ikiwa ni alama ya mapenzi au upendo kati yao.

Katika kukamilisha shamrashamra za ’siku ya wapendanao’, siyo kitu cha ajabu kuona kwenye baadhi ya maduka yauzayo kadi za matukio mbalimbali pamoja na maua kwa jina maarufu kama ’stationeries’ kuanzia tarehe za mwanzoni mwa mwezi Februari watu wakijivinjari kwa kununua vitu mbalimbali kulingana na mada ya ’wapendanao’. Utashuhudia makundi ya vijana pamoja na watu wazima wakichagua aina nzuri za kadi kwa maana ya maneno na maua ili wapate kuchagua moja wapo inayomfaa mpenzi au mpendwa wake kwa ajili ya kuadhimisha “Siku ya Wapendanao” au “Valentine Day”.

Kadi za heri ya siku ya ‘Wapendanao’ huandamana pamoja na maua mazuri ya waridi . yenye rangi ya wekundu. Wakati mwingine wapenzi au washabiki wanaojua kuadhimisha vema siku hiyo hutumiana hata zawadi mbalimbali ikiwa kama kumbukumbu kwa siku hiyo na mapenzi makubwa waliyonayo.

Majumba ya mengi ya starehe na kumbi za burudani bila kusahau hoteli hasa zile maarufu kwa pamoja hawako nyuma katika kuhakikisha wanafanya kila kivutio ili kuweza kuwateka wateja lukuki wakati wa ’wapendanao’ ili kuweza kutoa burudani mwanana wakati mwingine vikiambatana na vyakula na vinywaji vya uhakika.


Siku ya wapendanao kama inavyojulikana haijafungamana na matakwa ya dini yeyote wala aina ya mtu umpendaye kwa wakati huo. Hii ina maana kuwa salamu za wapendanao unaweza kutuma kwa Mama au Baba yako mzazi, kaka, dada, mume, rafiki wa kiume au wa kike, watoto n.k.

Leo basi nilitaka sote pamoja tufahamu nini chanzo cha siku ya Wapendanao na ni kwa nini ikaitwa Valentine Day, badala ya kuendelea kushabikia bila kuelewa chimbuko la siku hiyo muhimu duniani kwa wale wote ‘wapendanao’, kwa mujibu wa makala zilizoandikwa Birgit and Roger pamoja na www.history.com.

Katika historia ya kanisa Catholic huko Rumi, miaka 2000 iliyopita inasadikiwa kuwa taifa hilo lilikuwa kwenye vita ambapo Rumi kama mataifa mengine walihitaji askari wa kutosha kwa ajili ya shughuli hiyo.

Ilikuwa ni karne ya tatu wakati nchi ya Rumi ambayo kwa wakati huo ilikuwa ikitawaliwa na mtawala Cladius wa pili ambaye alitoa hoja ya kuhitaji askari vijana waajiriwe kwa wingi kwa ajili kwenda katika mapambano.

Kwa imani aliyokuwa nayo wakati huo, Mtawala Cladius wa pili aliamini kuwa askari mwanaume kijana ambaye hajaoa huwa ni askari shupavu sana awapo katika mapambano ya vita. Hivyo basi, uongozi wa wakati huo ulipitisha amri ya kuwa vijana wote waliopo wajiunge na jeshi na iwe marufuku kwa kijana yeyote kuoa au kufunga ndoa ili waweze kushiriki kikamilifu katika kazi ya jeshi.

Baada ya amri hiyo kutolewa, raia wote walitii katika nchi ya Rumi. Ilikuwa ni uamuzi mzito sana hasa kwa vijana. Lakini kama tujuavyo, panapokuwa na jambo zito kama hilo si ajabu kwa binadamu kama tujuavyo kuanza kuwa na mbinu mbadala. Nilazima kutakuwa na mambo ambayo yatajitokeza katika kuzuia au kukwamisha amri kama hiyo ili mradi tu kuwe na mpango fulani bila kujali kuwa ni wa kujenga au kubomoa usifanikiwe kwa asilimia fulani.

Basi alikuwepo Kasisi mmoja wa kanisa Katholic ambaye aliamua kuendelea na kufungisha ndoa kwa vijana lakini kwa njia ya siri sana. Kasisi huyo alijulikana kwa jina la Valentine au Valentinus na ilikuwa ni miaka kati ya 270 baada ya Kristo (270 AD).

Valentine alifanya kazi ya kufungisha ndoa kwa vijana wengi. Aliifanya kazi hiyo katika usiri mkubwa sana. Hivyo, siku jinsi zilivyokuwa zikisonga, mtawala Cladius alishangaa kuona vijana wengi aliowatarajia kuifanya kazi ya jeshi wengi wao walikuwa wameshafunga ndoa.

Jambo hili halikumpendeza kabisa Mtawala Cladius maana ilikuwa ni kinyume na matazamio na matarajio yake kutokana na amri aliyokwishatoa.

Siku zilivyozidi kwenda, siri hiyo iligundulika na Kasisi Valentine alikamatwa na kufungwa jela kwa kosa la kukiuka amri ya Mtawala wao. Alipokuwa kifungoni, kulikuwepo na makundi ya vijana ambao waliunga mkono huduma yake aliyokuwa anaitoa huduma kwa jamii, kwani waliamini kwa kufanya vile Father Valentine alikuwa akiwaokoa vijana wengi wakirumi kutokwenda kuishia jeshini. Vijana hawa walikuwa wakimtembelea mara kwa mara na kumtia moyo.

Historia inasema kuwa, katika watu hao pia alikuwepo binti mmoja ambaye Valentine alimpenda na siku moja kabla kesi yake haijatolewa hukumu Father Valentine alimwandikia barua binti huyo na mwishoni aliweka sahihi yake kama ‘Kutoka kwa Valentine’ au kwa lugha ya kiingereza tungeweza kusema ni ‘From your Valentine’ maneno ambayo mpaka leo yanatumika kama Valentine ni mpendwa au mpenzi wako.

Hali hii inadhihirisha kuwa, Fr. Valentine ndiyo aliyekuwa mtu wa kwanza kuhamasisha jamii kuendelea kupeana salamu za upendo kwa kila mmoja na kuita kuwa ni salamu za Valentine. Hivyo basi Fr. Valentine ndivyo alivyokuwa, nay eye ndiye Muasisi wa siku ya wapendao.

Jambo lingine la muhimu, ni kufahamu kuwa kwa nini sherehe hizi zikachaguliwa ziwe zinafanyika mwezi wa Februari katika tarehe za katikati ya mwezi huo, hii ni kwa sababu Fr. Valentine baada ya kuhukumiwa alipokuwa kifungoni, hukumu yake ilikuwa ni kunyongwa, na alinyongwa katika majira hayo hayo ya katikati ya mwezi Februari hiyo ndiyo sababu ya kuweka tarehe 14 Februari kuwa ni siku ya ‘Wapendao’ au ‘Valentine Day’ kwa kuzingatia kuwa mwezi February una siku kati ya 28 au 29 tu.

Vilevile, inahisiwa kuwa mbali na siku ya wapendanao kuhusishwa moja kwa moja na Fr. Valentine, vilevile hii ni siku ambayo mazao ya nafaka ambayo ni chakula kizuri kwa watu wengi wakati huo ndio majira ya uvunaji na upandaji wa mazao mbalimbali katika nchi ya Rumi (Roman).

Pia wapo waliokuwa wakisema kuwa, mwezi Februari umetambulikana kama ni ‘Siku ya Wapendanao’ katika nchi yetu na kwingineko, kwani wakati huo huwa ipo aina Fulani ya ndege jike huwa ndiyo majira yao ya kukutana na ndege dume. Ambapo hii hudhihirisha kuwa tarehe 14 ya mwezi wa pili ni siku ya wapendanao na kwa wale wenye kuwakumbuka wazazi wao ama ndugu wa karibu.


Nchi kama Uingereza, tarehe 14 Februari ya kila mwaka kuanzia karne ya 17 na 18, pia huadhimisha siku ya ‘Wapendanao’, kwa wapenzi na wachumba. Jambo hili lilianza kuzoeleka kidogo kidogo na baadaye kuweza kujengeka katika nchi ya Rumi yote na baadaye kusambaa kidogokidogo.

Siku za mwamzoni, watu wengi walikuwa wakitumiana salamu hizi kwa kuandikiana barua, ambapo baadaye kidogo kwenye karne ya kumi na nane hali hiyo ilianza kwisha na kuingia kwa Kadi maalumu ambapo zinakuwa zimejaa katika maduka mbalimbali pamoja na maua ya kupeana kwa wale wapendanao. Na sasa baada ya teknolojia kuongezeka salamu zinatumwa mno kwa njia ya text meseji za kwenye simu za kiganjani.

Tafiti mbalimbali zimeonyesha kuwa karibia kadi za Valentine bilioni moja zilikuwa zikinunuliwa na kutumwa sehemu mbalimbali hapa duniani, hii inafanya kuwa ni sikukuu kubwa ya pili duniani kwa watu kutumiana kadi, sikukuu ya kwanza ni X-mass ambapo inakisiwa karibu kadi zipatazo bilioni 2.6 hutumwa sehemu mbalimbali za dunia katika kutakiana heri ya X-mass.

Aidha, imegundulika kuwa, pamoja na wanunuzi au waandalizi ya shughuli hii kuwa wengi, lakini inakisiwa kuwa asilimia 85 ya washabiki wa masuala hayo ni wanawake.
Kwa ufupi kutokana na ufafanuzi huu, angalau wengi twaweza kufahamu nini kinajiri katika suala zima la Valentine Day.

Namalizia kwa kusema, maadhimisho ya ‘Siku ya Wapendanao’ yaanzie katika familia zetu, majirani zetu na hata makazini. Waandishi wa habari tupendane wenyewe kwa wenyewe ikiwa kama ishara ya kudumisha nia na malengo ya kazi zetu katika kuielimisha jamii. Happy Valentine Day!!!!

gladym@hotmail.com
www.gladnesshemedi.blogspot.com
www.ngajilanag.blogspot.com

No comments:

Post a Comment